MAANA HALISI YA UKRISTO BY DOMINICK MWENDA


 Sehemu fulani hivi alisikika mama mmoja akijibu kwa ujasiri mkubwa mara baada ya kuulizwa swali; kwanini unamtumikia Mungu? Nafikiri wewe ungekuwa na chakujibu, ungejibu vipi? Mama huyu akaanza kwa kusema; ikiwa na mtumikia MUNGU ili niende mbinguni na anipeleke motoni, Ikiwa namtumikia MUNGU ili nisiende motoni, na nipelekwe motoni; lakini ikiwa na mtumikia MUNGU kwa vile anastahili kufanyiwa hivyo na nipelekwe mbinguni. Majibu haya yalimridhisha muuliza swali. Je, jibu lako lingekuwa nini, je linakinzana na hili alilolijibu huyu mama?


Wengi wanaenda makanisani kusali ili wafu wao au wao wenyewe wazikwe kwa heshima ya kiibada, ili waonekane na wao wa pamoja na wale wanaowasaidia, ili kuficha maovu yao, ili kumaliza shida zao walizonazo, ili waonekane ni watu wema, ili wafiche makucha yao. Bila kutupilia mbali vijana; ili kupata wenza makanisani kwa unafiki wa kujifanya wana kondoo kumbe ni mbwa mwitu wa kali. Siipingi mitazamo hii huenda ni mizuri; ila haifai mbele za MUNGU. Je wewe unaenda kusali ili nini? 


Jaribu kuvuta picha, upo na jirani yako, naye hukusalimia pale anapohitaji tu msaada wako, na wakati haitaji msaada wako hana muda wewe! Mtu wa namna hii utamchukuliaje? Ni rafiki au ndugu au jirani kweli? 


Hizi ndizo imani zetu zilivyo. Kwa sababu ya matendo ambayo taifa la MUNGU lilikuwa likiyafanya kipindi cha nabii Isaya; Mungu aliamua kuwaeleza taifa lake wazi wazi juu ya ni mtu gani atakayemwangalia [atakaye mpa upendeleo/kipaombele]; akasema “maana vitu hivi vyote mikono yangu imeviumba, Hivyo vyote vikapata kuwako, asema Bwana; Lakini nitamtazama mtu huyu, aliye mnyenyekevu, mwenye roho iliyopondeka, atetemekaye asikiapo neno langu” Mungu anataja sifa tatu ndani ya mtu ambaye huwa anampenda na humpa kipaombele,

SIFA YA KWANZA

Mnyenyekevu au mpole; mtu aliye mnyenyekevu ni yeye, ajishushaye, wala hajikwezi. Akifanya kitu kizuri, basi utukufu wote ni wa Bwana; akipewa sifa za uongo, hayupo tayari kuzichukua; hutafuta kwanza heshima ya jina la Yesu; ni mtu wa upendo mwenye roho nzuri, humsaidia kila mtu aliyekatika shida bila kujali ikiwa mtu huyo atakuja amsaidie baadaye ama la! Huo ndio unyenyekevu. Je wewe ni mnyenyekevu?


SIFA YA PILI

Mwenye roho iliyopondeka. Mtu mwenye roho iliyopondeka ni mtu mwenye usafi wa moyo. Asiyemwongo, asiye mzinifu, asiye mwasherati, asiyekuwa shoga, asiye natamaa mbaya, mwenye roho ya kiasi[self-contol](kiasi maana yake ni uwezo wa kujizuia kwenye mambo fulani hususani mabaya, mfano kiasi katika uzinifu, humaanisha uwezo wa kujizuia kufanya uzinifu), aliyejaa matendo mema, mvumilivu, mcha Mungu, mwenye hekima ya kimungu na si ya kibinadamu, aamuaye kwa busara wala si kwa ukali, au upendeleo. Achukuaye shida ya jirani yake kama yake mwenyewe. Je mtu huyu ni wewe?


SIFA YA TATU

Atetemekaye asikiapo neno la mungu. Biblia inaposema atetemekaye asikiapo neno la MUNGU humaanisha, asiye lichukulia neno la MUNGU kama maneno mengine, anayelijua neno la MUNGU na kulishika kama ipasavyo, aliyetayari kumtangaza YESU kristo kwa saburi wala si kwa mabishano, asiyetumia neno la MUNGU vibaya, anayeliheshimu jina la YESU maana ndilo NENO lenyewe. Je, wewe upo kwenye kundi hili?

Umeshaanza kugundua kuwa haustahili hata kusikilizwa na Mwenyezi MUNGU katika shida zako. Mungu akusikilizaje, wakati haushiki maelekezo yake? Aliye pamoja na MUNGU hushika maagizo yake. Haieleti mantiki kusema kwamba unakipenda kitu alafu hukithamini.


Watu wengi leo wameufanya ukristo (imani) kuwa kama vazi tu! Leo yupo kwa MUNGU, kesho hayupo, bila sababu ya msingi! Haishangazi maana MUNGU anasema; Nayajua matendo yako, ya kuwa hu baridi wala hu moto; laiti (bora) ungelikuwa baridi au moto! Basi kwa kuwa u vuguvugu, wala hu moto wala hu baridi, nitakutapika utoke katika kinywa changu [Ufunuo 3:15-1]6. je wewe ni moto, baridi? Au vuguvugu? Bwana aliyasema maneno haya akiyaambia mataifa na kuwakataza mno. 

Jambo linalowatesa wakristo waliowengi ni hili; kuuzoea wokovu. Hapa ndipo imani hufa! Kuhubiri sana hata kuona hakuna haja ya kuandaa masomo, wala kipindi! kuimba sana na kuona hakuna haja ya kujiandaa! kutoa sana sadaka nakuona hakuna haja ya kuiombea! Kuhudhulia sana kanisani na kuona hakuna uzito wowote kwenye ibada [kwenda kanisani kwa mazoea]! kuishi sana kwenye wokovu, na kujiona ameumaliza mwendo! je na wewe unakabiriwa na mambo hayo? Chukua hatua ya kubadilika! Huu ndio ukawaida wenyewe;

Ulikuwa unahudhulia kila ibada, sasa haufanyi hivyo, unaona kunauzito;

Ulikuwa unaomba sana, sasa kama vile majukumu yamekulemea, huombi!

Ulikuwa na shauku kubwa ya kumtafuta Bwana lakini sasa haipo tena.

Kumtafuta Mungu kwenye matukio tu! Sherehe, misiba, au changamoto fulani!

Hizo ni ishara za ukawaida kukuwinda au kukuingia. Chukua hatua! 

Wengi tunamwabudu MUNGU kwa midomo tu! Kama maandiko ya semavyo waziwazi; Watu hawa huniheshimu kwa midomo yao, bali mioyo yao iko mbali nami. Nao waniabudu bure [Mathayo 15:8-9]. Je, wewe ni miongoni mwao? Kisa cha Yesu na mama msamalia pale kisimani kwenye kitabu cha Yohana sura ya nne; kinakupa funzo gani hasa unaposoma kuwa; Lakini saa yaja, nayo ipo, ambayo waabuduo wa kweli watamwabudu Baba kwa roho na kweli; maana Baba awatafuta watu kama hao wamuabudu [Yohana 4:23]? Swali; unamwabudu Mungu katika roho na kweli; au ni mhudhuliaji tu wa kanisani kama mwanamke alivyomuuliza Yesu kuwa wapi ni sehemu nzuri ya kuabudia kati ya Yerusalemu na Mlimani. Hii ni ishara ya kuabudu usichokijua! [Yohana 4:20-21]. Umeyaona hayo? Kuza imani yako!

Bila kipingamizi unakubaliana na mimi kuwa hizi ni nyakati za mwisho; Soma Mathayo 24:1-13, 2 Timotheo 3:1–5, 1 Timotheo 4:1–2, 2 Petro 3:3–10, nk. Kwa kukubaliana na mimi sasa twende tuchunguze maneno ya kinabii yaliyowahi kusemwa na nabii isaya; soma isaya 4:1-4. Rudia mara ya pili kuisoma. Sasa tuichambue!

Isaya 4:1; Na siku ile wanawake saba watamshika mtu mmoja[mwanaume, man], wakisema, Tutakula chakula chetu wenyewe, na kuvaa mavazi yetu wenyewe; lakini tunaitwa tu kwa jina lako; utuondolee aibu yetu.

Sawasawa na maandiko unaposikia mwanamke kinabii huashiria kanisa; mwanaume huwezakumaanisha kuwa ni Yesu kristo; Soma; Ufunuo 19:7–8, 2 Wakorintho 11:2, na Ufunuo 17:1–6. sehemu zote hizo hutoa dhana ya kuwa mwanamke ni kanisa au mfano wa watu ambao wanamtazamia bwana, kwa usahihi[mwanamke bikira], au kwa uongo [mwanamke kahaba]. Pia, namba 7, ni namba inayoonesha ukamilifu wa jambo; yaani; idadi kubwa, wingi au ukubwa wa kitu kwa kiwango cha juu. Tunapopata maana ya maneno haya; twaweza kupata tafsiri yake kiroho zaidi. Kwa lugha nyepesi maneno hayo yangesemwa hivi; itakuwa siku za mwisho ambapo; watu wengi(wanawake saba) watamfuata Yesu Kristo(mwanaume mmoja) wakisema, kwenye mambo yote tutafanya wenyewe bali sisi tuitwe tu kwa jina lako(wakristo) isije aibu yetu ikaonekana. umeanza kupata picha kuwa, jamii ya sasa inaigiza tu ukristo ili kuficha mabaya yake, na sio kuishi kwa usafi kama bibi harusi wa kristo kweli kweli. Huu ulikuwa ni utabiri wawakati wa mwisho. Utaniuliza nimejuaje! Unapoendelea kusoma mbele yake kwenye aya ya pili; biblia inasema; Siku ile chipukizi la Bwana litakuwa zuri na tukufu, na tunda la nchi litakuwa lenye fahari na uzuri kwa waliokoka wa Israeli. Hapa Biblia inataja tumaini jipya kwa wale waliokuwa wema kwa Mungu kwamba wataokoka. Hivyo kwa kuwa aya hii huongelea habari za mwisho, kadhalika na aya ya kwanza huelezea habari za mwisho vile vile. Umeliona hilo? Je wewe ni miongoni mwa hao wanawake saba(watu) wanaomwendea mwanaume mmoja(Yesu Kristo) wakitaka kuitwa tu kwa jina lake(Wakristo), lakini hawamtegemei yeye, ili waifiche aibu yao?

Ukiwa unasoma maandishi haya katika msisitizo wa kiroho, utagundua kuwa; kumtumikia kwetu MUNGU kwa namna tunayoendelea nayo si njema sana ikiwa nasi tu miongoni au mfano wa wanawake saba.


MAMBO YA KUZINGATIA ILI KUKUZA IMANI.

Haileti mantiki, kuendelea kujenga nyumba ikiwa kunakitu huibomoa kila siku unapoijenga. Ili uendelee haina budi kukiondoa kwanza kile kilichokikwazo, kisha ndipo usonge mbele!


#JAMBO LA KWANZA.

Kutoukubali ukawaida. Ukatae kila siku ukawaida asije Bwana akakutapika utoke katika kinywa chake! Soma Ufunuo 3:15-16.


#JAMBO LA PILI.

Tunza utakatifu hata kwenye hali nzuri au mbaya. Ukiwa katika hali nzuri mtukuze Bwana katika roho na kweli yote huku ukiomba akutunze katika huo uzuri; ukiwa kwenye hali mbaya, mtukuze MUNGU katika kweli yote; huku ukiomba akusaidie utoke katika mabaya hayo!


#JAMBO LA TATU.

Jiandae kiroho na kimwili kila siku unapokwenda kumlingana BWANA.hapa, kumbuka kuwa na moyo wa shukrani kwa Bwana, roho iliyopondeka, mnyenyekevu, na mtii kwa neno lake. Ikiwa ni mhudumu; jiandae kwa maombi,ili utukufu wa Bwana uonekane juu yako, wala usije kuaibisha kazi ya MUNGU kama wana wa skeva.soma Matendo ya Mitume 19:13–16.


#JAMBO LA NNE!

Jifunze kuisikiliza sauti ya Bwana. Mungu ni roho;Yohana 4:24. huongea na watu wake katika roho. Shida yetu ni kwamba tunaenda kwa MUNGU tukisubiri aongee kwa namna ya kimwili. Hautamsikia! Na hii ndiyo sababu ya kushindwa kutimiza mapenzi ya Mungu. Jaribu kufikiri, ikiwa umeshawahi kuishi eneo ambalo kuna mbwa au kondoo zaidi ya mmoja; uonapo mbwa anapiga kelele au anabweka, huona kama anakusumbua, anakuondolea burudiko ndani yako. Sivyo? Lakini kwa Mbwa mwenyake huona yakuwa wanawasiliana. Nini kinafanya tofauti hii? Ni kwamba wewe haupo kwenye ulimwengu(realm) wa mbwa au kondoo huyo. Kadhalika nasi tunapokuwa katika ulimwengu wa kimwili (physical realm) na kwenda kwa MUNGU aliye katika ulimwengu wa kiroho (spiritual realm) tunaona kama haeleweki, anatupigia kelele. Hivyo njia nzuri ni kwenda kiroho ikiwa kweli unataka kumsikia Mungu akisema na wewe.umeliona hilo?


#JAMBO LA TANO

Utayari wa kiinjili. Hapa nazungumzia kuwa tayari kuipeleka injili kwa wote waijuao na wasioijua. Soma 1 Petro 3:15“Bali mtakaseni Kristo kuwa Bwana mioyoni mwenu; siku zote mwe tayari kumjibu kila mtu awaulizaye habari za tumaini lililo ndani yenu; lakini kwa upole na kwa hofu.”umeliona hilo? 


#JAMBO LA SITA.

Kuwa mwombaji anayeomba! Kwa kulielewa kipengele hichi vyema soma nakala yangu inayoitwa, TUMIA MAOMBI KUJENGA UFALME WA MUNGU DUNIANI. Usiwe mwombaji kwa kuwa upo kwenye shida! Kuomba iwe tabia, na sehemu ya maisha yako. Kwa maana imetupasa kuomba kila siku bila kuchoka.


#JAMBO LA SABA. 

Zingatia utu wako wa ndani na wanje. Haijarishi upoje, bali kile ukitendacho kwa nje ndicho kiujazacho moyo wake; ikiwa ni matusi basi ndani yako yamejaa matusi ikiwa ni wema basi ndani mwako kumejaa wema. Kumbuka hatuwezi kuona upepo, bali tunaweza kutambua uelekeo wake kwa kile ukifanyacho. Vilevile; Roho mtakatifu hujidhihirisha kwa matendo mema katika mwili wako, vilevile, Roho mwovu hujdhirisha kwa matendo maovu kupitia mwili wako. Roho yule umpaye nafasi ndiye hujidhihirisha kwako. Hivyo, ukristo wetu, na neema yetu ianze kuonekana kwanjia nje hata ndani pia; tuvae mavazi ya staha, na heshima, mfano wa watoto wa MUNGU na si wana wa ulimwengu. Lugha nzuri, ukarimu, kubariki na si kulaani; kuwasaidia walio dhaifu, na kuwatia moyo walio katika mapito magumu. Chochote tukifanyo tufanye kama watoto wa MUNGU. MUNGU huwapenda watu wa namna hii!

Mwishowe, tujue kuwa, shetani huyaambia mataifa leo hii kuwa, sio tatizo kama unamwamini MUNGU ama la! Mbinguni ni nyumbani kwetu, ishini vile mtakavyo! Na hivi wengi sana wanamwamini MUNGU ila wanaishi kama watakavyo wao na si kama atakavyo MUNGU! Je wewe ni miongoni mwao? Tumtafute Bwana wetu bila kuchoka. 

YouTube; YouTube https://share.google/MUWArBsQFKMvvtEkY

TikTok; https://www.tiktok.com/@dominick_mwenda

Instagram;https://www.instagram.com/mwl.dominickmwenda

Audiomack; https://audiomack.com/dominick mwenda

Email;    dominickmwenda99@gmail.com

WhatsApp; https://wa.me/255614236148

UBARIKIWE KIWE SANA

Comments

Popular posts from this blog

SIRI NYETI KUHUSU MAHUSIANO BY DOMINICK MWENDA

TRUST IN GOD'S TIMING BY ERICA BROWN edited by DOMINICK MWENDA

DOMINICK MWENDA : THE PRESTIGE OF BEING WITH GOD