VITA KATI YA NURU NA GIZA ##THE BATTLE BETWEEN LIGHT AND DARKNESS BY DOMINICKMWENDA
Je, umewahi kukutana na watu kama hawa?
Je, yamkini hawa wameishindwa ile vita ya kiroho?
Biblia ilikuwa inamaanisha sana iliposema kwenye 1 Wakorinto 10:12 Kwa hiyo anayejidhania kuwa amesimama na aangalie asianguke.
Mungu aliiumba dunia kama upanuzi[expansion] na mwendelezo[extension] wa ufalme wa mbinguni katika namna ya kimwili. Akaumba mwanadamu aliyekatika namna ya kimwili ili autawale ulimwengu huo kiroho! Hivyo, Mwenyezi Mungu alifanya hivyo ili aabudiwe kama mbinguni wanavyomwabudu. Ndio maana watu hukusanyika kwa ibada! Shetani naye akaona ni vyema na yeye kuanzisha utaratibu kama huu, wakuabudiwa katika ulimwengu huu huu! Sasa, ndani ya dunia hi, shetani naye alianzisha kanisa lake litakalokuwa likipiga vita dhidi yakanisa la kweli la MUNGU. Umeliona jambo hilo? Hapa ndipo naanzia!
Mambo yakuyajua juu ya vita ya kiroho.
Ili tuweze kupigana vita hii, ni lazima tujue wigo wake. Hakuna dakika, saa au siku itakayopita pasipokuwindwa na nguvu za giza ili kukudondosha hapo ulipo. Daudi alitoka tu nje auangalie ufalme wake, shetani akamweza kwa kumpa tamaa [Soma 2 Samweli 11:2]. Petro alimsaliti Yesu, hata maratatu! Hii ilikuwa ni dhambi, sema alijutia dhambi yake kisha akasamehewa! Soma [Mathayo 26:69-75]. Hivyo, humu humu katika maisha ya kila siku shetani kaweka mitego. Tunapoongea na marafiki, tunapokutana kwa ibada, tunapofanya kazi zetu na nk. Kama kijana ni bora kuelewa maana vijana ni rasilimali[asset] kubwa sana. Usipotumika kwa MUNGU, utatumika na Ibirisi. Twende tuchunguze baadhi ya mambo kadhaa!
#jambo la kwanza.
Wewe ni askari katika roho.
Mara unapoamua kumfuata Yesu KRISTO si kama watu wa mataifa wanavyomwendea basi ni lazima ujue ya kuwa wewe ni askari. Ukizubaa utawezwa na mwovu. Soma kitabu cha waefeso 6:10-20 kwa msisitizo wa kiroho. Paulo anataja sifa kadhaa za askari wa kiroho, anasema; twaeni silaha zote za MUNGU; silaha hizi ni upendo, utuwema, ukarimu, kiasi, uvumilivu, unyenyekevu, ukweli na hekima(aya ya 10-15); pia kama askari yabidi aitwae ngao ya imani ambayo ni jina la YESU, kisha aitwae chepeo ya wokovu na upanga wa roho ambao ni neno la MUNGU, kwa sala zote na maombi, akisali bila kuchoka na kukesha kwa jambo hilo (Waefeso 6:16-18). je, umeona vile ambavyo askari wa KRISTO yambidi awe? Je wewe ni askari wa Kristo? Unavigezo hivyo?
#jambo la pili
Askari hodari ni yule anayeshinda dhambi na majaribu. Kiukweli, dhambi huonekana ni tamu sana kwa macho, lakini ni mbaya sana mithili ya pipi yenye sumu ndani! Ukiishinda dhambi bado tutakuita askari! Tatizo hapa ni kwamba, watu wengi sana leo huigiza ya kuwa wao ni watu wema, lakini sio hata kidogo. Acha tulione hili vizuri. Unaacha kwenda kukutana na MUNGU wako, kwa sababu ya kukwazana na mtu! Je, wewe ni askari kweli? Kisa maneno tu yanakukimbiza kanisani!je, wewe ni askari kweli? Umeambiwa tu ukweli, unaona umehukumiwa na mwanadamu! Je, wewe ni askari kweli? Askari wa KRISTO yupo tayari kila muda kupambana katika roho, na wala hatishwi na mambo yakumtoa katika njia ya kweli. Sasa tuikimbie dhambi, turudi tukatubu maana Bwana asema “… wewe u mnyonge, mwenye mashaka, maskini, kipofu na uchi. Nakupa shauri ununue kwangu dhahabu ilyosafishwa kwa moto, upate kuwa tajiri, na mavazi meupe upate kuvaa, aibu ya uchi wako isionekane, na dawa ya kupaka machoni pako upate kuona. Wote niwapendao mimi nawakemea na kuwarudi; basi fanya bidii, UKATUBU! [ufunuo 3:17-19]”. Ndugu yangu MUNGU anatuita kwenye toba, tumemkosea, tumetena dhambi! Kama sio sisi basi ndugu zzetu, au jirani zetu au jamaa zetu au rafiki zetu. Kwenye kikundi chenu toba inahitajika, kwenye biashara yako, taifa lako, familia yako, ukoo wako, maisha yako, wazazi wako; kote ombea toba!
#jambo la tatu.
Nguvu za giza zinautawala wake ndani ya dunia. Je, ulikuwa ukifahamu hivyo au ndio unasikia kwa mara ya kwanza? Kana mkuu wa giza aliyekabidhiwa katika mtaa wako unaoishi, yupo aliyekabidhiwa kijiji, mwingine kata, wilaya, mkoa, taifa na hata dunia!soma Waefeso 6:12; inasema vita vyetu si juu ya damu na nyama bali ni juu ya wakuu wa giza hili, majeshi ya pepo wabaya na juu ya falme na mamlaka. Hizi falme na mamlaka ndizo nizizungumziazo. Soma kitabu cha Danieli 10:12-14; inasema “ usiogope Ee Danieli, kwa maana tangu siku ile ya kwanza ulipotia moyo wako ufahamu, na kujinyenyekeza mbele ya MUNGU wako, maneno yako yalisikiwa; nami nimekuja kwa ajili ya maneno yako. Lakini mkuu wa ufalme wa Uajemi alinipinga siku ishirini na moja; bali tazama, huyo Mikaeli, mmoja wa hao wakuu wambele, akaja kunisaidia; nami nikamwacha huko pamoja na wafalme wa uajemi. Umeyasoma na kuyaelewa maneno hayo ambayo Malaika wa Bwana alikuwa akimwambia Danieli, juu ya falme ya giza ya uajemi na wakuu wake? Falme hizi zipo ili kuhakikisha huwezi kukua kiroho. Huleta magonjwa, ajali, umaskini, vita, na majaribu ili tu usiweze kuvuka. Wakati mwingine kukuchukiza kwa watu, au kukufanya uone watu wengine kuwa ni chukizo. Hizi zote ni kazi zake! Sasa, tupambane dhidi ya falme hizi za giza kama maaskari hodari na tuzishinde KATIKA JINA LA YESU. Soma pia 2 wakorinto 4:4.
#jambo la nne.
Shetani amewekeza duniani. Uwekezaji wake unahitaji wafanyakazi ambao ni wanadamu wakti huo huo MUNGU huitaji pia watenda kazi ambao ni wanadamu hao hao! Sasa, shetani anatumia starehe, miziki, utajiri, mikataba na maagano, vifungo na vizuizi, na kujikweza na majigambo ili watu wasijekupata utulivu wa kumtafakari BWANA. Watu wapo radhi kusimama dakika 90 kuangalia mpira lakini hawawezi hata kusimama dakika 5 kwa maombi. Watu wapo radhi kucheza miziki ya kiulimwengu hata kwa masaa matatu, lakini hawawezi hata kumwabudu MUNGU kwa dakika 10. je, umeona jinsi shetani alivyowanasa watu? Leo hii ukimuuliza mtu, akutajie wasanii watato wa nyimbo za kidunia, atakuzidishia hadi kumi; lakini ukimwambia akutajie mistari mitatu ya biblia, hata huo mmoja atautaja kwa shida sana. Umeliona jambo hilo? Tujifunze kumpendeza MUNGU!
#Jambo la tano
Sababu ya wanawake wengi kuonekana kufungwa na nguvu za giza ndiyo hii! Kama nilivyosema awali juu ya uwekezaji wa shetani; vilevile uwekezaji huu umeenda hata kwenye vitu visivyo vya kiasili ambavyo watu hivipenda sana. Na vitu hivi ni kama nywele za kusuka (yapo makampuni yaliyojiunganisha na hila za mwovu), mapambo mbalimbali na mavazi. Wanawake ndio wapenzi wa vitu hivi! Hapa najua si wote wawezao kulipokea neno hili; ila siwezi kuficha jambo nililosikia kwa masikio yangu na kuliona kwa macho yangu! Sasa, siwezi kusema kuwa hivyo vitu ni najisi, ila nasema kuwa mwenye hekima ya kimungu atavipokea kwa maombi na kuvunja maagano na mapatilizo yaliopo. Ni sawa si kila aina ya hayo mapambo yana nguvu hizo za giza, lakini ni kwamba wapo watu waliokamatwa na nguvu za giza kwa sababu zake. Ukiweza kulipokea neno hili, lipokee kwa shukrani. Nakupa ushauri; usije ukaona kwa sababu kuna mtumishi mkubwa wa MUNGU anafanya hivyo, nawe ukafanya; au ukaona ukifanya hakuna madhara na ukajihisi uko salama. Hapana! Jipambe si mfano wa watu wa dunia bali kama mtoto na mfuasi wa KRISTO.
#jambo la sita.
Vita ya kiroho ni pambano kuu kati ya nuru na giza. Watu huchagua wapi watasimama katika mapambano hayo. Kuukubali upande mmoja ni kuuvamia upande mwingine na kuutupilia mbali. Maana kati ya nuru na giza hakuna uhusiano wowote. Umechagua nini maishani mwako? Nuru? Au giza?
Kwa kuhitimisha naweza kusema kwamba yapo mengi sana katika ulimwengu wa kiroho. Na ni watu wachache sana wanayotambua mambo hayo. Jaribu kuzingatia haya niliyokwambia, kisha yapime kama yataleta mabadiliko kwenye maisha yako.
Makala hii imeandikwa na kuhaririwa na DOMINICK MWENDA.
Usiache kufuatilia makala nyingine hapa hapa katika blog yetu.
Acha comment Yako hapo kama swali kisha nitarijibu
Nipo mtandaoni
YouTube; GLOPEC TV/DOMINICK MWENDA
Tiktok&instagram; dominick_mwenda
Blog;glopecnetwork.blogspot.com
Email; dominickmwenda99@gmail.com
Glopecnetwork1@gmail.com
Mobile numbe; +255 614 236 148
© dominick mwenda
.png)
Comments
Post a Comment